Tuesday, 3 December 2013

BAJETI YA KUWAHUDUMIA ALBINO. Halmashauri Zaagizwa











Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Hawa Ghasia ameziagiza Halmashauri zote Nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuzingatia takwimu za sensa ya mwaka 2012.

 
Mhe. Hawa Ghasia aliyasema hayo katika maadhimisho ya Nane (8) ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) Tanzania yalifanyika mkoani Singida ambapo Mhe. Hawa Ghasia alikuwa mgeni rasmi. Kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni Saratani ya Ngozi, Je Waijua?
“Halmashauri zote Nchini zitenge bajeti ili kuwahudumia Albino wote katika maeneo yao, waweze kupata mafuta ya ngozi pamoja na huduma nyingine. Wafanye hivyo kwa kuzingatia takwimu za sense mpya ya mwaka 2012.” Alisema Mhe. Hawa Ghasia.
Mhe. Hawa Ghasia aliwaomba watu wenye Albinism kujitokeza mara kwa mara kupima hali za afya zao na kupata ushauri wa kitaalam wa namna ya kulinda na kuimarisha afya za ngozi na kuwahi kufika Hospitali kupatiwa matibabu ya haraka na mapema pale inapobainika kunyemelewa na tatizo la Saratani ili kunusuru vifo visivyo vya lazima na kuzipunguzia familia na Serikali gharama inazopata kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa Saratani.
“Madaktari Bingwa wamethibitisha kwamba maradhi ya Saratani ya ngozi yanatibika na kupona kabisa, endapo tatizo litatambulika na kuthibitika katika hatua za mwanzo. Kuchelewa kwenda Hospitali ni kuhatarisha maisha. Tukumbuke kuwa KINGA NI BORA KULIKO TIBA.” Alisema Mhe. Hawa Ghasia.
Aidha Mhe. Hawa Ghasia aliwaomba wananchi wote na Wadau wa maendeleo kuielimisha jamii na kuwasaidia watu wenye Albinism kulielewa tatizo la Kansa na kuwasaidia kuzifikia huduma za afya pale wanapokabiliwa na matatizo mbalimbali ya afya likiwemo tatizo la Saratani ya Ngozi na kuachana na imani potofu inayopelekea kutokea kwa mauaji ya Albino.
“Saratani ya ngozi ni maradhi yanayoweza kumpata mtu yeyote Duniani. Ni aibu kusikia kuwa eti mtu anafikiri anaweza kuwa tajiri akiwa na kiungo cha binadamu Albino; ni udhaifu wa kiimani iwe kwa mkristu ama mwislamu, hakuna dini inayoruhusu kuua binadamu wenzetu kwa sababu yoyote ile. Tunalitia Taifa letu aibu. Hebu tujielimishe na kuelimishana ili kuufahamu ugonjwa huu wa saratani ya ngozi na kuachana na imani potofu.” Alisema Mhe. Hawa Ghasia.
Vilevile Mhe Hawa Ghasia alisema Serikali itaendelea kuwashughulikia watu wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu kwa mujibu wa sheria na kuwaomba wananchi kote nchini kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mahakama kwa kuwafichua wahalifu hawa na kutoa ushahidi Mahakamani pale wanapotakiwa kufaya hivyo. Aliendelea kueleza kuwa wananch hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa vile Serikali imejizatiti katika kuhakikisha kwamba Raia wema wanalindwa kwa kutunza siri zote zilizopokelewa katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Kwa upande mwingine katika risala yao kwa Mhe. Hawa Ghasia, Chama cha Maalbino Tanzania kilitoa mapendekezo na maombi 11 kwa serikali ili kuondokana na changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni:
Waraka wa TAMISEMI unaoelekeza utekelezaji wa sera ya afya kwa watu wenye ulemavu kutibiwa bure utolewe pia na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika hospitali zote zilizoko chini yake na hata zile za binafsi zinazoshirikiana nazo, na jambo hili lisikawie kwani gharama za matibabu ikiwemo upasuaji ziko juu sana na watu wengi wanaendelea kuteseka na kupoteza maisha kila siku mijini na vijijini;
Waraka wa TAMISEMI haufahamiki na walio wengi hivyo Serikali ielimishe umma kupitia vyombo vya habari na pia walimu wote wa shule za Msingi
Wataalam wanaohitimu KCMC (RDTC) na kupelekwa katika hospitali za mikoa wawezeshwe kwa vifaa na vitendea kazi vingine ili waokoe maisha ya watoto, wanaume na wanawake yanayoteketea kwa saratani ya ngozi mijini na vijijini;
Serikali iweke mkakati maalum, wenye bajeti maalum, ili kukabiliana na tatizo la saratani ya ngozi ambayo imeendelea kutuua kabla ya uhuru na hadi leo na kufikia kuyafupisha maisha yetu kuwa miaka thelathini, tofauti na watanzania wengine na katika nchi nyingine duniani ambako watu wenye ualbino wana umri wa kuishi ambao ni sawa na watu wengine kwenye jamii;
Elimu juu ya ulemavu nchini, hususan elimu juu ya ualbino ifundishwe shuleni ili kujenga jamii inayojitambua na kupunguza unyanyapaa ambao ni changamoto kwa watu wenye ulemavu na familia zao;
Maadhimisho haya ni ya Nane(8) nchini Tanzania huku taarifa zikionesha kuwa Tanzania ni nchi pekee duniani inayoadhimisha Siku ya Ualbino na hivyo kuleta mjadala unaotaka kuwa na siku moja ya Afrika au Kidunia ambayo itasaidia kuongeza ufahamu zaidi wa jamii juu ya ualbino, ikifuatiwa ama kutanguliwa na Shirikala la Afya duniania (WHO) kutambua ualbino kama ulemavu.

No comments:

Post a Comment