Tuesday, 3 December 2013

Homa ya Ripoti ya CAG yatinga bungeni












Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza mkutano wake wa 14 mjini Dodoma leo, huku kukiwa na homa ya matokeo ya mjadala wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2011/12.


Taarifa hiyo inatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo sambamba na majibu ya awali ya Serikali kuhusu kasoro katika matumizi ya fedha za umma zilizobainishwa na CAG, huku Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zikitarajiwa kutoa taarifa ambazo zitakuwa mwongozo wa mjadala bungeni.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kuwa, kwa kawaida wabunge wanapaswa kujadili taarifa ya CAG kabla ya mkutano wa Bunge la Bajeti ambalo hufanyika Aprili, ili kuwawezesha kutoa maoni na maelekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika mwaka wa fedha unaofuata.
Kwa kuzingatia kalenda ya mikutano ya Bunge, mkutano wa 14 ulipaswa kufanyika Februari 2014, lakini kama Spika Anne Makinda alivyotangaza katika mkutano uliopita, unafanyika kuanzia leo ili kutoa fursa kwa Bunge Maalumu la Katiba ambalo litakaa kati ya Januari na Machi 2014.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema jana kuwa tayari Serikali ilishawasilisha majibu ya awali kuhusu hoja za ukaguzi na kwamba baada ya taarifa za LAAC na PAC kutakuwa na majibu ya nyongeza kwa hoja mpya zitakazoibuliwa na kamati hizo.
“Serikali tayari ilishatoa majibu ya awali sasa kwa sababu Kamati za PAC na LAAC zilikuwa zikikutana na watendaji wakuu wa Serikali ambao taasisi au wizara zao zilionekana kuwa na kasoro kwenye hesabu, tutawasikia watasema nini na hapo ndipo Serikali itatoa tena ya nyongeza,” alisema Lukuvi.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aliporidhia taarifa ya CAG kuwasilishwa bungeni kisha kujadiliwa na wabunge, baadhi ya vigogo wa Serikali wakiwamo mawaziri na watendaji wakuu ambao wizara na idara wanazoziongoza zilibainika kuhusika na upotevu mkubwa wa fedha za umma waling’olewa katika nafasi zao.
Katika mjadala wa mwaka jana, mawaziri sita na naibu mawaziri wawili walitimuliwa kazi, yakiwa ni matokeo ya mjadala mkali bungeni wa ripoti ya CAG ya 2010/2011. Mbali na vigogo hao, pia fagio hilo liliwakumba wakurugenzi wakuu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na yule wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu zilizoisukuma Serikali kupeleka bungeni marekebisho katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu ambavyo vilitafsiriwa kuwa vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya CAG.
Kwa maana hiyo, Bunge linajadili kwa mara ya kwanza ripoti ya CAG tangu marekebisho ya sheria hiyo yanayozuia Bunge kujadili ripoti ya CAG kabla Serikali haijajibu hoja za ukaguzi, yapitishwe bungeni Februari mwaka huu.
Operesheni tokomeza
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inatarajiwa kuwasilisha taarifa kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanza Oktoba 4 mwaka huu ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kabla ya kusitishwa na Serikali Novemba Mosi.

No comments:

Post a Comment