Dar es Salaam.Vita ya kuwania urais katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imeingia katika sura mpya baada ya Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kumlalamikia mrithi wake katika wadhifa
huo, Edward Lowassa akimtuhumu kumfanyia mbinu chafu
.
.
Huku akinukuu habari iliyoandikwa na gazeti hili
Septemba 16, 2013 yenye kichwa cha habari, ‘Lowassa afichua siri ya
mradi wa maji Ziwa Victoria’, Sumaye alisema Lowassa amekuwa akimfanyia
propaganda na mbinu chafu.
Katika habari hiyo, ambayo Lowassa alialikwa
katika Harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT huko
Kahama, Shinyanga hivi karibuni, alikaririwa akisema mawaziri watatu, tu
ndiyo waliounga mkono wakati alipopendekeza kutekelezwa kwa mradi huo
kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri cha Serikali ya Awamu ya Tatu
iliyokuwa chini ya Benjamin Mkapa.
Lowassa, ambaye katika kipindi hicho alikuwa
Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, aliwataja mawaziri waliounga
mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sumaye
Alisema hizo ni mbinu chafu zilizokuwa na lengo la
kumpaka matope… “Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi
wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli
kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi
umetekelezwa chini ya uangalizi wangu,” alisema na kuongeza:
“Kama Waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi
mkubwa hivyo peke yake, akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma?
Mbona hata bado kuna kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya
maji?” alihoji Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika
Serikali ya Awamu ya Tatu.
Alipotafutwa kwa simu kuelezea madai hayo,
Lowassa, ambaye yuko Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, alisema hawezi
kubishana na Sumaye kwa kuwa anamheshimu kwani amewahi kuwa kiongozi
mkubwa serikalini.
“No comment’ (sina la kusema), siwezi kubishana na
Sumaye kwani amewahi kushika nyadhifa za juu katika nchi hii,” alisema
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Sumaye alimtuhumu Lowassa kwa kusema uongo na kuongeza kuwa amefanya kosa la jinai kutoa siri za Baraza la Mawaziri.
“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo
mkavu, mhusika kama waziri mwandamizi wakati huo na sasa anawinda nafasi
kubwa katika nchi, hakutegemewa kutoa siri za Baraza la Mawaziri, labda
amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayosema siyo ya kweli,
vinginevyo ni kosa la jinai na akishtakiwa anafungwa jela,” alisema.
Sumaye alisema hizo ni mbinu chafu zinazofanywa dhidi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment