Dar es Salaam. Washiriki
mbalimbali wa maendeleo na wadau wa masuala ya jinsia wametakiwa
kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia vinafikia tamati.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki wakati akizindua siku 16 za
kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Sambamba na uzinduzi huo Kairuki alizindua pia
mfumo wa utoaji wa huduma kwa mfumo wa One Stop Center ambao unajumuisha
huduma zote muhimu kwa watakaokutana na ukatili wa kijinsia kama vile
polisi, afya na ustawi wa jamii kutolewa sehemu moja.
Alisema licha ya kuwa vitendo hivyo vimekuwa
vikiongezeka kila kukicha, ni asilimia 4 tu ya kesi hizo ndiyo
huripotiwa katika vyombo vya sheria hali inayochangia wahusika kuendelea
kuwa huru mitaani.
“Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali
katika kuhakikisha vitendo hivi vinatokomezwa, lakini wanawake ambao kwa
kiasi kikubwa ndiyo wamekuwa wakinyanyasika hawakimbilii kutafuta
msaada wa kisheria” alisema Kairuki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake
katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Naomi Kaihura
alisema licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kupinga vita vitendo
vya ukatili, changamoto kubwa inabaki katika upatikanaji wa fomu za
polisi ambazo hutoa kibali kwa muathirika kupata matibabu.
Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia
waathirika kupoteza maisha na wengine kukata tamaa ya kutoa ripoti
kuhusiana na ukatili waliofanyiwa.
“Ukiritimba katika upatikanaji wa PF3 ni
changamoto kubwa hali inayosababisha waathirika kupoteza maisha hata
kabla hawajapata matibabu,” alisema.
No comments:
Post a Comment