Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema wizara yake imewasimamisha kazi baadhi ya maofisa kutokana na kujihusisha na biashara haramu ya ujangili wa meno ya tembo.
Akizungumza baada ya kufungua warsha ya wadau wa
wanyamapori jana, Balozi Kagasheki alisema mapambano dhidi ya ujangili
yanakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kuhusisha mtandao mkubwa
ambao ndani yake kuna watu wazito na vigogo serikalini.
“Biashara hii wacha bwana, ni ngumu kwelikweli,
inahusisha mtandao mkubwa… tayari tumewasimamisha baadhi ya watumishi na
hivi karibuni nitayaweka wazi majina ya vigogo na watu wengine
wanaojihusisha na mtandao huu.
“Haitaishia kuwasimamisha kazi tu, hatua zaidi
dhidi yao zitachukuliwa kwani kujihusisha na vitendo vya ujangili ni
sawa na kuhujumu uchumi wa Watanzania,” alisema Balozi Kagasheki.
Hata hivyo, Balozi Kagasheki amekuwa akitoa ahadi ya kuwataja vigogo wanaojihusisha na ujangili bila kutekeleza.
Kauli hiyo ya Kagasheki imekuja zikiwa zimepita
wiki tatu tangu Rais Jakaya Kikwete kusitisha kwa muda Operesheni
Tokomeza, lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa Serikali kujipanga na
kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwenye awamu ya kwanza ya operesheni
hiyo.
Balozi Kagasheki alisema rushwa na kukosekana kwa
utashi wa kisiasa ndiyo sababu inayochangia kuwapo kwa changamoto kubwa
katika vita dhidi ya biashara hiyo haramu, inayohatarisha maisha ya
tembo na soko la utalii.
“Hii ni rasilimali ya Watanzania, hivyo hatutaweza kuvumilia watu wachache wanufaike,” alisema.
No comments:
Post a Comment