Rais Jakaya Kikwete ameiongezea tena muda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuiwezesha kumaliza kazi yake.
Tume hiyo ambayo ilitakiwa kumaliza kazi yake,
Desemba 15, mwaka huu itaendelea na kazi kuanzia Desemba 16 hadi Desemba
30, mwaka huu.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongezea
Tume hiyo muda wa kufanya kazi yake. Baada ya maombi yake ya kwanza,
Rais Kikwete aliiongezea Tume hiyo siku 45 kuanzia Novemba Mosi hadi
Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya kuomba kuongezewa muda, ilitakiwa kukamilisha kazi yake kesho.
Rais Kikwete ameiongezea Tume hiyo muda zaidi kwa
mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza Tume
hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa sheria inampa Rais mamlaka
ya kuiongezea tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku 60.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku
nyingine 14, Rais Kikwete atakuwa ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59
kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Hatua hiyo ilitarajiwa hasa baada ya Tume hiyo
kusimamisha kazi zake kwa muda baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wake,
Dk Sengondo Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika
Kusini alikokuwa anatibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu
wasiojulikana nyumbani kwake Novemba 3, mwaka huu.
Baada ya kifo hicho, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alitangaza kusitishwa kwa muda
shughuli za Tume hiyo.
Kifo cha Dk Mvungi, ambaye aliteuliwa kwa tiketi
ya Chama cha NCCR-Mageuzi kilikuwa pigo kwa Tume hiyo kwani mwanasheria
huyo alikuwa amebobea katika masuala ya katiba.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotolewa Juni 4, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment