Geita.Rais Jakaya Kikwete jana aligoma kupokea zawadi ya dhahabu kutoka
Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema viongozi
wa kampuni hiyo walitaka kumkabidhi Rais Kikwete gramu 227 za dhahabu
safi wakati alipotembelea mgodi huo.
Rais Kikwete badala yake aliwaelekeza waiuze dhahabu na fedha zitakazopatikana zitumike kuwasaidia watoto yatima.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa sherehe ya
kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje kidogo ya mji
mdogo wa Kharuma ambao ni makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale,
Geita.
Gramu hizo 227 zina thamani ya Sh16 milioni kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete
aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu,
iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto
yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais
Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema umeongeza thamani ya
dhahabu na maisha ya wananchi katika eneo hilo... “Mmefanya vizuri na
mgodi huu, ni mradi wa maana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na
kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili
pongezi,” alisema Rais Kikwete.
Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio kwani unazalisha
dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulishafuliwa na kutoa dhahabu.
Ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa kiasi cha Sh 1.6 bilioni
kimewekezwa kuuendeleza.
Uongozi wa mgodi huo ulisema mgodi huo unaozalisha
kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi, na unaajiri watu 45 kati
yao wanawake 10.
Rais Kikwete alizindua mgodi huo ikiwa sehemu ya
kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake Geita ambao ni
moja ya mikoa minne aliyoianzisha mwaka jana. Mikoa mingine ni Simiyu,
Njombe na Katavi.
No comments:
Post a Comment