Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Full
Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amesema mawaziri mizigo ni
matunda ya uteuzi mbovu unaofanywa na mamlaka husika ambao hauzingatii
vipawa vya uongozi.
Pia ameonya ukabila na kuvitaka vyama vya siasa
vinavyodaiwa kuendeshwa kwa misingi hiyo vifutwe haraka kabla
havijachafua hali ya hewa. Akizungumza jana kwenye ibada ya Sikukuu ya
Krismasi iliyofanyika katika kanisa hilo Mwenge, Dar es Salaam, Askofu
Kakobe alisema si rahisi kwa mtu ambaye hana kipaji cha kuongoza akawa
kiongozi, kwani hataweza kumudu nafasi atakayopewa.
“Siku zote uongozi ni kipaji, sasa matatizo
yanayotukumba ya kuwa na viongozi mizigo ni kutokana na uteuzi mbovu
ambao hauangalii suala la vipaji vya watu,” alisema na kuongeza:
“Tumekuwa tukijichagulia tu viongozi tena kwa kuangalia maeneo
wanayotoka jambo ambalo siyo jema na la hatari, mifano hai tunaiona
sasa. Wanachokifanya viongozi mizigo ni kujihudumia wao na kuwatelekeza
wananchi ambao ndiyo wangekuwa wa kwanza kuhudumiwa.”
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM na Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye walitaja orodha ya
mawaziri wanaoelezewa kuwa mizigo. Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Christopher Chiza na Naibu wake Adam Malima.
Orodha hiyo iliongezeka baada ya Bunge kumtaja
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na Manaibu
wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama
wanatosha kusimamia wizara hiyo baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufichua ufisasi kwenye wizara hiyo.
Viongozi wanaotoa zawadi
Akizungumzia suala la viongozi wa kisiasa kutoa
zawadi kwa wananchi alisema ni hatari, kwani ipo siku watataka kurudisha
walichokitoa. Alisema wananchi wamekuwa wakirubuniwa kwa khanga,
vitenge, fulana na chakula cha siku moja ili kuwapa watu hao nafasi ya
uongozi, lakini baada ya hapo kinachofuata ni mateso, kwani wananyonywa
na maisha yanazidi kuwa magumu kwao.
“Viongozi wa kisiasa wamekuwa hatari, wanajitahidi
kutafuta uongozi kwa gharama yoyote ile, hasa kwa kuwarubuni wananchi
kwa kuwapa zawadi jambo ambalo si jema na mtu anayefanya hivyo hafai
kuwa kiongozi kwa taifa na mbele za Mungu,” alisema Askofu Kakobe.
Alisema wananchi wanatakiwa kuwakataa viongozi wa
aina hiyo, kwani hawana vipaji vya uongozi, bali wanatumia fedha
kutafuta nafasi wanazozitaka na kwamba wakipata watawatelekeza kwa
kurudisha walichokitoa.”
Ukabila.
Akizungumzia ukabila, Askofu Kakobe alisema miaka
ya nyuma taifa lilikuwa halina vitendo vya ukabila, lakini kwa sasa hali
imekuwa mbaya, kwani unaonekana waziwazi.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa nchini vimekuwa
vikidaiwa kuendeshwa kikabila, huku sheria za nchi zikikataza... “Kama
kuna chama cha siasa kinaendeshwa kikabila kifutwe haraka, kwani ni
hatari kwa nchi na taifa kwa jumla.”
No comments:
Post a Comment